Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Akizungumza katika hitimisho la Mkutano wa 39 wa Kitaifa wa Wakuu wa Idara za Elimu, Aref alisema kufikia lengo hilo kunahitaji kuanza kufundisha teknolojia ya akili bandia kuanzia shuleni, pamoja na kuwaandaa wanafunzi kuwa wabunifu, watafiti na viongozi tangu miaka ya mwanzo ya elimu.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Elimu pamoja na wakuu na manaibu wao kutoka mikoa yote 31 ya Iran kupitia njia ya mkutano wa video.
Aref alisema walimu ni miongoni mwa makundi yenye ushawishi mkubwa katika kujenga mustakabali wa nchi, akieleza kuwa ustaarabu wa Iran wenye historia ya maelfu ya miaka pia umejengwa kupitia mchango wa walimu wa nchi hiyo katika vipindi mbalimbali vya historia.
Akikumbuka mashahidi wa Shule ya “Shajareh Tayyibeh” mjini Minab, kusini mwa Iran, Aref alisema tukio hilo lilikuwa miongoni mwa sababu muhimu za kushindwa kwa Marekani na Israel katika vita vya Ramadhani. Alilaani tukio hilo na kusema hakuna sababu inayoweza kuhalalisha uhalifu huo.
Aref pia alikosoa ukimya wa wanaodai kutetea haki za binadamu kuhusu kile alichokiita uhalifu wa Israel na Marekani huko Gaza na Iran, akisema ukimya huo umeacha doa la kudumu katika ustaarabu wa Magharibi.
Elimu haiwezi kuendelezwa kwa amri pekee
Naibu huyo wa kwanza wa Rais alisema sayansi, elimu na malezi haviwezi kuendelezwa kwa kutumia kauli za jumla na amri pekee. Alisisitiza kwamba kuinua kiwango cha kielimu cha wanafunzi hakutafikiwa kwa amri ya Waziri wa Elimu pekee, bali kunahitaji mashauriano, kubadilishana mawazo na mijadala ya kisayansi.
Alisisitiza pia kwamba malezi ndiyo msingi wa elimu, hivyo mipango ya muda mrefu inapaswa kuwekwa katika sekta ya elimu na malezi, huku akipendekeza programu za sekta hiyo ziwe za muda usiopungua miaka 10.
Aref alisema mwanafunzi anapaswa kuanzia darasa la kwanza kulelewa katika mazingira yanayomjengea uwajibikaji, ubunifu, utafiti na udadisi, pamoja na kuelewa kwa usahihi misingi ya kisayansi na kihisabati ili kusaidia kuongeza uzalishaji nchini.
Iran itashikilia haki zake kuhusu usimamizi wa Mlango wa Hormuz
Akizungumzia hali ya nchi baada ya vita, Aref alisema Iran imeingia katika hatua mpya na itaendelea kushikilia haki zake pia katika suala la usimamizi wa Mlango wa Hormuz.
Alisema Iran si nchi inayotafuta vita, lakini ina uwezo mkubwa wa kujilinda.
“Sisi si wafuasi wa vita, lakini ni wapiganaji wenye nguvu. Ikiwa adui atafanya kosa na kutushambulia, atapata jibu litakalomfanya atetemeke kila atakaposikia jina la Iran.”
Aref alisema Iran imefanikiwa katika vita viwili vya hivi karibuni katika nyanja mbalimbali, ikiwemo uwanja wa mapambano, jamii, huduma, diplomasia, sayansi na teknolojia.
Iran kulenga kuwa miongoni mwa nchi 10 bora kwa akili bandia
Aref alisisitiza tena kwamba teknolojia zinazoibukia na akili bandia si chaguo tena, bali ni hitaji muhimu kwa mustakabali wa nchi.
Kwa mujibu wa Aref, Iran inapaswa kuweka mpango wa kuingia katika orodha ya nchi 10 bora duniani katika sekta ya akili bandia, huku elimu ya teknolojia hiyo ikianza tangu shuleni. Alisema hatua za awali za utekelezaji wa mpango huo tayari zimeanza.
Aidha, alisema serikali imedhamiria kuendelea kutekeleza hati ya mageuzi ya elimu na malezi, kuboresha hadhi na maisha ya walimu, pamoja na kuhakikisha haki na usawa katika upatikanaji wa elimu.
Aref alisema kuhifadhi na kuimarisha mtaji wa kijamii ni miongoni mwa mikakati ya kipaumbele ya serikali, huku sekta ya elimu ikiwa na nafasi muhimu katika kufikia lengo hilo.
Alisema mkakati wa adui ni kuchochea mgawanyiko wa kijamii, wakati mkakati wa serikali ni kuimarisha uwezo wa Iran wa kustahimili changamoto za kiuchumi na kijamii.
Kwa msingi huo, alisisitiza kwamba taasisi za kisayansi, kielimu na malezi zinapaswa kuwa huru dhidi ya mitazamo ya kisiasa, huku masuala ya malezi katika shule yakifuatiliwa kwa umakini zaidi.
Mwisho, Aref alieleza kwamba Rais wa Iran anaweka umuhimu mkubwa katika sekta ya elimu na kumuomba Waziri wa Elimu kuandaa mpango mkakati wa muda mrefu kwa kipindi cha baada ya vita, ukiweka msisitizo maalumu katika ustaarabu wa Iran, kuendeleza lugha ya Kiajemi kuwa lugha ya kisayansi, pamoja na kuimarisha maendeleo ya kisayansi ya nchi.
Maoni yako